Kwa mujibu wa taarifa ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Seneta Raja Nasir Abbas Ja‘fari, Rais wa Baraza la Umoja wa Waislamu Pakistan, alisema katika taarifa yake: uvamizi wa Marekani dhidi ya Venezuela ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa, Mkataba wa Umoja wa Mataifa, na kanuni zote zinazokubalika duniani. Kuzingirwa kiuchumi na mashinikizo ya kijeshi dhidi ya nchi hiyo kunafichua uso halisi wa sera za kichokozi na kibeberu za serikali ya Trump; sera ambazo, badala ya diplomasia na mazungumzo, zinatanguliza maslahi ya mafuta na jitihada za kupotosha fikra za umma ili kuficha kushindwa kwa ndani.
Aliongeza kuwa: kuonesha nguvu za kijeshi za Marekani nje ya mipaka yake, kwa hakika ni jaribio lililoshindikana la kuficha udhaifu wa uongozi na migogoro ya kisiasa ya ndani ya nchi hiyo. Njia hii si tu haisaidii utulivu wa dunia, bali huzidisha mvutano na kuusukuma ulimwengu kuelekea kwenye ukosefu mkubwa wa usalama.
Rais wa Baraza la Umoja wa Waislamu Pakistan pia alizitaja kauli za uchochezi za Donald Trump dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni mfano wa wazi wa sera za viwango viwili na unafiki, na akasisitiza kuwa: kuzungumza kuingilia masuala ya ndani ya nchi huru kwa kisingizio cha kuunga mkono maandamano, kutoka kwa mtu mwenye historia ndefu ya kukandamiza wapinzani na kuchochea vurugu, si chochote ila ni unafiki wa wazi.
Alibainisha kuwa: misimamo ya aina hii ni tishio kubwa kwa amani ya dunia, na haina lengo jingine isipokuwa kuonesha nguvu na kufanya propaganda za kisiasa binafsi; ilhali madai ya kupokea Tuzo ya Amani ya Nobel yanageuka kuwa mkanganyiko wa wazi na usioaminika.
Seneta Nasir Abbas Ja‘fari, mwishoni mwa taarifa yake, alitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa, hususan Umoja wa Mataifa na taasisi za kimataifa za haki za binadamu, kutonyamaza kimya mbele ya uvamizi wa Marekani, bali badala ya kutumia nguvu, waimarishe njia ya mazungumzo, majadiliano na diplomasia. Aidha alisisitiza kuwa dunia haina tena uwezo wa kuvumilia vita vipya, na kukabiliana na malengo ya kibeberu ni jambo la dharura. Pakistan na mataifa yote huru na yanayojitegemea yanapaswa kusimama bega kwa bega na nchi zilizodhulumiwa, na kwa ajili ya kutetea amani duniani, uhuru wa kitaifa wa nchi, na ubora wa sheria za kimataifa, yawe na sauti moja iliyo imara na yenye nguvu.
Maoni yako